Serikali imesema itatoa mwongozo kuhusu wachezaji wa kigeni watakaoruhusiwa kusajiliwa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara hivi karibuni, imeelezwa
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema ni lazima uandaliwe utaratibu wa kuruhusu wachezaji hao wa kigeni ambao unalenga zaidi kukuza vipaji vya nyota wazawa.
Mwakyembe alisema serikali haitakubali kuona wachezaji wasiokuwa na viwango wanasajiliwa na klabu za hapa nchini kwa sababu uamuzi huo unawanyima nafasi wachezaji Watanzania ambao wanaibukia.
"Ukiruhusu kila mchezaji aje, hatutakuza vipaji vya vijana wetu wanaochipukia kila mwaka, tutatoa uamuzi hivi karibuni, sisi ndio tunaotoa vibali, lazima tuwe na vigezo, sio tukubali tu, tutajadiliana ili kufikia uamuzi utakaokuwa na faida kwetu," alisema Mwakyembe.