Wakati Yanga ilipotoa majina ya wachezaji wanaoanza mchezo dhidi ya Azam Fc, wengi walishtuka kumuona winga Deus Kaseke akipangwa namba mbili badala ya Juma Abdul ambaye alikosa mchezo huo kwa kuwa na kadi tatu za njano
Hata hivyo kile alichofanya Kaseke katika nafasi hiyo, kiliwafurahisha wengi akiwemo kocha wa zamani wa Yanga Hans van Pluijm ambaye alimwagia sifa kedekede
Pluijm ambaye alikuwepo uwanjani kushuhudia mtanange huo, alisema anamfahamu vizuri Kaseke kuwa ni mchezaji makini ambaye hufuata maelekezo anayopewa na walimu wake
"Namfahamu vizuri Kaseke, nimefanya nae kazi Yanga na kule Singida United. Ni mchezaji ambaye ukimuelekeza jambo uwanjani, atalifanya inavyopaswa. Hata nilipomuona anacheza namba mbili, sikushangaa," alisema
Naye mshambuliaji wa zamani wa Yanga Amissi Tambwe amesema kiwango kilichoonyeshwa na Kaseke akicheza namba mbili kilimshangaza
"Sikuwahi kumuona Kaseke akicheza namba mbili, nimeshangaa, kwani alionesha kuimudu nafasi hiyo kama huwa anacheza kila siku," alisema Tambwe ambaye bado anaamini siku moja atarejea Yanga
Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Taifa na kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana, Kaseke alionyesha uwezo mkubwa wa kupanda na kushuka pengine kama ataendelea kutumika katika nafasi hiyo, anaweza kuwa bora zaidi