Kikosi cha mabingwa wa kihistoria Tanzania, Yanga jioni ya leo mishale ya saa kumi kamili, kitashuka kwenye uwanja wa Taifa kuumana na Azam Fc ukiwa ni mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Baada ya kumaliza ratiba ya mechi za mikoani, leo Yanga inaanza ratiba yake ya mechi nne katika dimba la Taifa wakianza na wana rambaramba hao
Mara nyingi mechi zinazowakutanisha miamba hao huwa hazitabiriki, Azam Fc imekuwa na kawaida ya kutoa upinzani mkali kila inapokutana na Yanga
Leo Yanga inahitaji ushindi ili kupanda kwenye nafasi ya pili inayoshikiliwa na Azam Fc
Katika mchezo huo, Yanga itakosa huduma ya beki wake kisiki Lamine Moro ambaye anatumikia adhabu ya mechi tatu baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania
Lakini pia mabingwa hao wa kihistoria hawatakuwa na huduma ya nahodha Papy Tshishimbi ambaye bado ni majeruhi
Mkongwe Kelvin Yondani ambaye katika mechi mbili zilizopita alitumika kama kiungo, leo huenda akarejeshwa katika eneo lake la ulinzi
Viingilio vya mchezo huo VIP A - 15,000/-, VIP B&C - 10,000/-, MZUNGUKO - 5,000/-
Pia unaweza kununua jezi ya Yanga Tsh 20,000/- kupitia maduka ya GSM kisha ukajipatia tiketi ya mzunguuko bure pamoja na jarida