Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dk.Hassan Abbasi, amethibitisha klabu ya JKT Tanzania haitaruhusiwa kuingiza mashabiki uwanja wa Jamhuri Dodoma baada ya kukiuka taratibu za afya ambazo zimewekwa na serikali kwa wananchi kukaa umbali wa mita moja na nusu baina ya mtu mmoja na mwingine pindi wawapo katika viwanja vya michezo pamoja na katika shughuli mbalimbali ikiwa ni hatua za kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona
Uwanja huo jana ulifurika mashabiki waliojitokeza kwa wingi kuwashuhudia mabingwa wa kihistoria Yanga ambao walishuka dimbani hapo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne
Pamoja na Serikali kuchukua hatua kutokana na ukiukwaji huo, uwanja wa Jamhuri pia umelalamikiwa kuwa sehemu yake ya kuchezea 'pitch' ni mbovu na ni hatari kwa afya za wachezaji
Baadhi ya wadau wameonyeshwa kushangazwa na hali ya uwanja huo hasa ikizingatiwa uko Makao Makuu ya nchi
Pengine hii ni nafasi kwa TFF kwa kushirikiana na Wamiliki wa uwanja, kufanya maboresho ya eneo la kuchezea