Mchezo wa ligi kuu ya Vodacom kati ya JKT Tanzania dhidi ya Yanga ambao umepigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, umemaliza kwa timu hizo kugawana pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1
JKT Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Michael Aidan kwenye dakika ya 37 baada ya kumchungulia mlinda lango wa Yanga Metacha Mnata ambaye alikuwa amesogea mbele ya lango lake
Yanga iliyotawala mchezo huo kwa muda mwingi, ililazimika kusubiri mpaka dakika ya 77 kusawazisha kupitia kwa Patrick Sibomana PS ambaye alimalizia kwa kisigino mpira uliotemwa na mlinda lango wa JKT Tanzania, Abdulrahman Mohammed baada ya shuti la Haruna Niyonzima

Yanga ilikuwa na wakati mgumu kuipenya ngome ya JKT Tanzania ambao walicheza kwa kujihami huku wakitumia mashambulizi ya kushitukiza

Wakati mchezo huo ukielekea ukingoni, Yanga ilipata pigo baada ya beki wake kisiki Lamine Moro kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya mchezo mbaya sambamba na kiungo wa JKT Tanzania Mwinyi Kazimoto
Matokeo ya leo yanaibakisha Yanga katika nafasi ya tatu baada ya kufikisha alama 55
Mchezo unaofuata ni dhidi ya Azam Fc, Juni 21 katika uwanja wa Taifa