Beki mpya wa kushoto wa Yanga, Eric Rutanga, anatarajiwa kuzoa kitita cha zaidi ya shilingi milioni 270 ndani ya mkataba wake wa miaka miwili Jangwani.
Rutanga ni mmoja wa wachezaji waliopo katika faili la Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael ambaye amependekeza wasajiliwe kwa udi na uvumba.
Beki huyo msimu uliopita alitakiwa na Yanga, lakini ilishindikana kutua Jangwani kutokana na kubanwa na mkataba wake ndani ya klabu ya Rayon Sports ya Rwanda
Licha ya hivi karibuni kutajwa kusaini mkataba wa awali na klabu ya Polisi ya Rwanda, inaelezwa GSM wamefanya kweli kuhakikisha fundi huyo anatua Jangwani kuungana na kocha Luc Eymael ambaye amemuhitaji sana
Kutokana na kiwango chake, hasa umahiri wake wa kukaba na kupanda kusaidia mashambulizi, Eymael anaamini beki huyo atawasaidia katika mpango wake wa kusuka kikosi cha mauaji cha msimu ujao.
Habari kutoka ndani ya Yanga na mtu wa karibu na mchezaji huyo, amelidokeza gazeti la Bingwa kuwa kati ya fedha hizo, dau la usajili ni Shilingi milioni 81, huku mshahara wa mwaka wake wa kwanza wa mkataba ukiwa ni Shilingi milioni 83.
Kiasi kikingine cha fedha atakazopata mchezaji huyo ni Shilingi milioni 111, zikiwa ni mshahara wake wa mwaka wa pili kutegemea na kiwango atakachokionyesha Jangwani.
Mtoa habari huyo wa uhakika, alisema:
"Tunashukuru tumefanikiwa kumalizana na Eric, dau la usajili ni Dola za Marekani 35,000 (sh mil. 81) na mshahara wake kwa mwaka wa kwanza wa mkataba ni Dola 3,000 (sh mil. 6.9) kwa mwezi na mwaka wa pili atalipwa Dola 4,000 (Sh mil 9.2) kwa mwezi"
Kwa mshahara wa Sh. milioni 6.9 kwa mwezi, kwa mwaka wa kwanza, mchezaji huyo atapokea Sh. milioni 82 na mwaka unaofuatia itakuwa ni Sh. milioni 9.2 mara 12 ambayo ni sawa na shilingi milioni 110, hivyo kufanya jumla ya zaidi ya Sh. milioni 270 pamoja na dau la usajili.
Akizungumzia dili hilo, Wakala wa mchezaji huyo ambaye ni raia wa Ivory Coast anayeishi Afrika Kusini, Herve Tra B, alisema kuwa amefarijika kuona wamemalizana na Yanga ikibakia kutua nchini kusaini mkataba.
"Nitoe shukrani zangu kwa uongozi wa Yanga na Kmapuni ya GSM kwa kufanikisha dili hili ambalo naamini litakuwa na manufaa makubwa kwa Yanga na mchezaji mwenyewe"
"Yanga ni timu kubwa Afrika, hivyo ni fahari kubwa kwa mchezaji kama Eric kuichezea na ninaamini atafika mbali"
"Uzuri tayari Yanga kuna wachezaji wakubwa kutoka Rwanda ambao ni Haruna Niyonzima na Patrick Sibomana, hivyo Eric ni kama atakuwa nyumbani kwa kuungana na ndugu zake hao," alisema Meneja huyo"
Akimzungumzia Rutanga, Eymael alisema: "Ninamfahamu vizuri sana Eric, ni mchezaji mzuri akiwa anaichezea timu ya Taifa ya Rwanda, ndio maana nilimtaka nikifahamu atakuja kutusaidia msimu ujao"
Mbali ya Rutanga, wachezaji wengine wapya waliopo katika orodha ya wanaotakiwa Yanga kwa ajili ya msimu ujao ni Tuisila Kisinda wa AS Vita, Mpiana Mozizi (FC Lupopo), Ally Niyonzima (Rayon Sports), Heritier Makambo (Horoya AC, Guinea) na wengineo.
Wazawa ni Bakari Mwanyeto (Coastal Union), Novatus Dismas (Biashara United), David Luhende (Kagera Sugar), Reliant Lusajo na Blaise Bigirimana (Namungo), Yassin Mustafa, Sixtus Sabilo (Polisi Tanzania) na wengineo