Kiungo mshambuliaji wa Yanga Bernard Morrison amesema Simba 'wamemganda' wakimlazimisha ajiunge nao baada ya kumpa fedha 'kishika uchumba'
Morrison amekiri kupokea dola 5,000 (zaidi ya Tsh Milioni 10) kutoka kwa Bosi wa Simba zikiwa ni ushawishi ili ajiunge nao
"Nilipojiunga na Yanga, kutokana na mambo niiyokuwa nimesikia kuwa timu hailipi mishahara, nilipanga nisiongeze mkataba. Tayari nilikuwa nimeanza mazungumzo na vilabu vya Orlando Pirates na Cape Town City mpango wangu ukiwa kurejea Afrika Kusini," alifunguka Morrison
"Ndipo wakati huo viongozi wa Simba walinitafuta wakinitaka nijiunge nao ili niwasaidie kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao"
"Walimtuma wakala wao ambaye alikuja kunishawishi na kunikabidhi dola elfu tano, ili nisaini mkataba wao. Aliniambia fedha hiyo imetoka kwa Rais wa Simba na amesema ananihitaji sana kwenye timu yake," aliongeza Morrison
"Kwa kuwa nilikuwa katika mazungumzo na vilabu vingine pia, nikawaambia wanitumie nakala ya mkataba wao WhatsApp ili niuone kabla ya kuanza majadilinao lakini hawakufanya hivyo, wakamtuma mtu akauleta moja kwa moja kwangu"
"Sasa wananisumbua baada ya kusikia taarifa kuwa nimeongeza miaka miwili Yanga. Yule mtu waliyemtuma amekuwa akinisumbua sana kutokana na fedha waliyonipa"
"Mimi sikuomba pesa yoyote kutoka kwao, ni wao wenyewe walionipa, nafikiria kuwarudishia pesa yao kutokana na usumbufu wao"
Morrison alifichua sakata hilo kwa kiongozi mmoja mwandamizi wa Yanga pia akiomba ushauri kwa kiongozi huyo
Morrison aliongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Yanga ambao utaanza mara baada ya mkataba wa awali wa miezi sita utakapomalizika Julai 31