Yanga imeanza kwa kishindo ngwe ya lala salama ligi kuu ya Vodacom baada ya kuichapa Mwadui Fc bao 1-0 katika mchezo mkali uliopigwa uwanja wa CCM Kambarage
Mabingwa hao wa kihistoria waliuanza mchezo huo kwa moto mkali na walihitaji dakika sita tu kupata bao lao kupitia kwa Mapinduzi Balama 'kipenseli'
Ilikuwa krosi ya Jaffary Mohammed iliyounganishwa vyema na Ditram Nchimbi kisha mlinda lango wa Mwadui kuokoa shambulizi hilo na mpira kumfikia Deus Kaseke ambaye alimtengea Balama aliyeachia fataki lililojaa kimiani
Kikosi cha Yanga leo kilionyesha utofauti mkubwa ukilinganisha na walivyocheza wiki iliyopita na kupoteza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC
Kipindi cha kwanza Yanga walikuwa bora kuliko wapinzani wao huku Mwadui Fc wakifanya vizuri katika kipindi cha pili lakini wakashindwa kuipenya ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya beki kisiki Lamine Moro na Said Juma Makapu huku mkongwe Kelvin Yondani akicheza juu yao akichafua mipango yote ya Mwadui Fc
Yanga ilifunga bao ambalo lilikataliwa kwenye kipindi cha pili mfungaji Ditram Nchimbi akidhaniwa kuotea
Ushindi huo umeifanya Yanga ifikishe alama 54 sawa na Azam Fc, timu hizo zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa
Mchezo unaofuata ni dhidi ya JKT Tanzania ambao utapigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma


