Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amefichua kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Luc Eymael atakapofika Shinyanga, ataitisha kikao cha pamoja kati ya wachezaji na benchi la ufundi pamoja na suala la mshambuliaji David Molinga ili kubaini kilichotokea na kupelekea nyota huyo akabaki jijini Dar es salaam
Molinga alikuwa tayari ameondolewa kwenye mipango ya mchezo dhidi ya Mwadui Fc ambao utapigwa kesho Jumamosi baada ya kushindwa kusafiri na timu juzi
Hata hivyo Eymael ameuomba uongozi wa Yanga aende nae kwani anaamini mchango wa nyota huyo bado unahitajika
"Ni kweli tukio la Molinga kuachwa Dar lilisababisha sintofahamu na mengi kusemwa, hata hivyo kocha ameomba aende nae na kile kilichotokea atakwenda kufahamu hukohuko," amesema
"Molinga bado ni mchezaji wetu na amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu yetu, nadhani kama kocha ameamua kwenda nae ni jambo zuri"
Nyota huyo hakuondoka na timu juzi kwa kile alichoeleza kutojumuishwa katika msafara na kocha Mkwasa licha ya uongozi wa Yanga kuthibitisha kuwa Mcongomani huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji waliopaswa kusafiri