Jana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2020-21 alikumbushia goli lilivyofungwa na Bernard Morison dhidi ya Simba na kulifananishana mkuki wa sumu kali
Wakati akimalizia kusome Bajeti hiyo Bungeni, Dodoma, Waziri Mpango alisema, Rais John Magufuli alipokwenda kushuhudia pambano hilo la watani wa jadi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika Job Ndugai na Naibu wake Dk Tulia Ackson walichezwa na machale kwa kutokwenda uwanjani kushuhudia Simba ikipoteza pambano hilo.
"Naamini hamjasahau siku Mhe. Magufuli alipokwenda uwanja wa Taifa kujionea mpambano wa watani wa jadi Yanga na Simba na kushuhudia mnyama akipigwa mkuki mmoja wa sumu kali na Benard Morrison! Inaonekana Mheshimiwa Waziri Mkuu, na wewe Mheshimiwa Spika na hata Mheshimiwa Naibu Spika machale yaliwacheza mapema siku hiyo hamkuonekana uwanjani!!," alisema Dk Mpango
Kwa mara nyingine, Morrison ameendelea kujizolea umaarufu na heshima ya kipee kwa kile alchokifanya March 08, baada ya kuifungia Yanga bao la ushindi katika mchezo ambao, pamoja na kushuhudiwa na Rais wa nchi Dk John Magufuli, pia ulishuhudiwa na Rais wa TFF Wallace Karia na Rais CAF Ahmad Ahmad