Wakati mwingine ni vyema kwa kiongozi kuwa na busara. Kuna mambo huwa hayapaswi kufanyiwa utani, kwani yanaweza kupelekea kuamsha hisia za watu na kusababisha madhara
Yanga na Simba ni vilabu wapinzani na watani wa jadi kwa miaka mingi. Vilabu hivi tofauti yao iko uwanjani tu, nje ya uwanja Yanga na Simba ni ndugu wanaosaidiana na kuzikana
Tunafahamu Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara hutumia muda mwingi kuitania, kuikebehi na hata kuikashifu Yanga pale inapokumbana na changamoto
Wanayanga wamemzoea kwa kuwa wanafahamu, ni mtoto wao, alizaliwa ndani ya nyumba ya Mzee Sunday Manara 'computer' ambaye ni Mwanayanga
Lakini juzi Manara alivuka mipaka kwani alifanya utani kwa tukio ambalo kwa kweli halikupaswa kufanyiwa utani
Haikuwa sahihi kufanya utani na tukio la ajali ambalo msafara wa Yanga ulipata mkoani Singida wakati wakielekea Shinyanga kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu
Ilikuwa ni ajali mbaya ambayo ingeweza kuwa na madhara makubwa, baada ya basi kupasuka tairi la mbele lakini ashukuriwe Mwenye ez Mungu kwa kunusuru yasitokee madhara kwa wachezaji na wote waliokuwa katika msafara ule
Ajali haina kinga, kufanya utani na jambo hilo ni sawa umefurahia kile kilichotokea bila ya kujali madhara ambayo yangesababishwa na ajali hiyo
Kumekuwa na sauti inasambaa kwenye mitandao ya kijamii yenye maneno makali ya Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli ambaye ni miongoni mwa waliokerwa sana na kile alichofanya Manara
Bumbuli alikuwa miongoni mwa abiria katika basi la Yanga hivyo anafahamu ni kwa kiasi gani Mwenye ez Mungu aliwanusuru na kifo
Na hapa ndipo tunapotilia mkazo, kuna masuala mengine hayapaswi kufanyiwa utani hata kidogo kwani yanaweza kuamsha hisia za watu
Ifike wakati klabu ya Simba imdhibiti Msemaji wake kwani anakoelekea anaweza kuja kusababisha matatizo makubwa
Viongozi wa Yanga nao wanapaswa kuzungumza kuhusu hili, kuendelea kunyamaza ni kumpa Manara uhalali wa kuendeleza hicho anachofanya kwa kudhani yuko sahihi
Hata vyombo vya habari ambavyo vinampa Manara 'Air Time' wanapaswa kujitafakari. Maana inakuwaje Msemaji wa klabu ya Simba mnamuita kwenye mahojiano azungumzie klabu yake lakini muda mwingi anatumia kuizungumza Yanga na bado mnaendelea kumpa nafasi?
Nadhani ni vyema sintofahamu iliyojitokea sasa ikatumika kuchora mstari ambao utaendelea kuzifanya Yanga na Simba kudumisha utamaduni wa utani ambao hauwezi kuathiri undugu wetu