Uongozi wa Yanga umekusudia kukisuka upya kikosi chake kurejesha heshima ya timu hiyo msimu ujao
Kipigo cha mabao 3-0 kutoka KMC juzi, kimekoleza moto kuelekea maboresho ya kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, zimedokeza kuwa, Yanga kwa kushirikiana na wadhamini/wahisani wao GSM, wiki hii watakamilisha usajili wa nyota watatu wa kigeni, baadhi ya wachezaji hao ikielezwa tayari wako njiani kuja kusaini mikataba
Moja ya mambo ambayo yamewatibua mabosi wa Yanga ni kitendo cha baadhi ya wachezaji kutozingatia program za mazoezi waliyoachiwa na kocha Luc Eymael wakati wa mapumziko ya corona
Kuna wachezaji wamerejea mazoezini wakiwa hawako fiti huku wengine wakiongezeka uzito kwa kiwango cha kutisha!
Mcongomani David Molinga yeye alitia fora kwa kuongezeka kilo 12 akifuatiwa na Yikpe Gnamien ambaye aliongezeka kilo 10
Taarifa za ndani zimebainisha kuwa ni nyota watano tu wa kigeni ambao huenda wakanusurika katika mkakati huo wa kuisuka upya Yanga
Nyota hao ni mlinda lango Farouq Shikhalo, Lamine Moro, nahodha Papy Tshishimbi, Bernard Morrison na Haruna Niyonzima
Kwa upande wa wachezaji wazawa, nyota wasiozidi kumi wanaweza kubakia kutegemea na mapendekezo ya kocha Eymael ambaye ametaka kufanya mchujo kupitia mechi zilizobaki kwenye ligi
Mmoja wa mabosi wa Yanga ameeleza kutofurahishwa na kitendo cha wachezaji kutozingatia maelekezo wanayopewa na tayari wamewapa taarifa kuwa panga litawahusu
"Kocha alitoa program ya mazoezi kwa wachezaji wote, lakini inaonekana kuna ambao hawakuwa wakizingatia na majibu yake tumeyapata katika mchezo wa jana (juzi dhidi ya KMC). Ninachoweza kuwaambia Wanayanga, wasiumie sana, wasubiri mwalimu arejee tukisuke upya kikosi chetu. Msimu ujao watafurahi tu," alifunguka mmoja wa viongozi wa Yanga katika mahojiano na gazeti la Bingwa
Katika mchezo huo dhidi ya KMC, ukiwa ni wa kwanza tangu shughuli za michezo ziliporuhusiwa baada ya kusimamishwa kutokana na hofu ya kuenea kwa maambukizi ya virus vya corona, wachezaji wa Yanga walionekana kuwa wazito mno tofauti na wa wapinzani wao.