Uongozi wa klabu ya Yanga pamoja na wachezaji wameweka mkakati wa kuhakikisha wanashinda mechi zote 11 zilizobaki na kufikisha alama 84 ambazo zitawahakikishia kumaliza nafasi ya pili au pengine hata kutwaa ubingwa kama mambo yatakwenda 'mrama' kwa watani zao Simba
Aidha mabingwa hao wa kihistoria wameweka mpango wa kuhakikisha wanashinda taji la FA ili kukata tiketi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao
Juzi Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla pamoja na viongozi waandamizi w aklabu hiyo, wakiongozana na wadhamini wao GSM, walizungumza na wachezaji kuweka mkakati huo wa kumaliza msimu kibabe
Kikao hicho kilichodumu kwa takribani masaa matatu, kiliweka mkakati huo kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye kila mchezo
Inaelezwa GSM wametoa ahadi kubwa, wataendelea kutoa zile posho za kila ushindi huku wakiahidi kuongeza uzito wa 'furushi' wanalotoa
Aidha, mmoja wa wachezaji amefichua kuwa wameahidiwa kitita cha Tsh Milioni 50 kama watafanikiwa kutinga fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho (ASFC)
Nae Afisa Mhamasishaji na Msemaji wa klabu ya Yanga Antonio Nugaz amesema pamoja na kutopewa nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu, hawajakata tamaa
Nugaz amesema mpango mkakati wao wa kukusanya alama 84 unaweza kuwapa ubingwa
"Simba hajawa bora kiasi cha kujihakikishia hawawezi kufungwa katika michezo 10 iliyobakia, tunajua atateleza tu sehemu na hiyo ndiyo itakuwa nafasi yetu. Bado ubingwa upo wazi na hatujakata tamaa hadi pale watakapofikisha alama ambazo hatuwezi kuzifikia," alisema
Kimahesabu SImba itahitaji kushinda michezo mitano kati ya 10 iliyobaki ili kutetea ubingwa waliotwaa kwa misimu miwili iliyopita