Kiungo mshambuliaji wa Yanga Bernard Morrison amesema walisubiri na sasa wako tayari kurejea uwanjani baada ya Serikali kuruhusu michezo kuendela nchini kuanzia Juni Mosi
Mghana huyo aliyejitengenezea jina Yanga ndani ya muda mfupi, amesema wakati umefika wa kuwapa furaha mashabiki wake ambao alikuwa amewakumbuka sana
"Nimefurahi kurudi uwanjani, 'nimemisi' mashabiki wangu kwa kipindi kirefu, naahidi kurudi kwa kasi ili kuipa ushindi timu yangu," alitamba Morrison
Nyota huyo aliyetua mwezi Januari akitokea klabu ya DC Motema Pembe, amesema ametumia vyema kipindi chote ligi ilipokuwa imesimama kufanya mazoezi hivyo anaamini hakutakuwa na changamoto yoyote kwa upande wake kurejea uwanjani
"Nimefuata kwa umakini maelekezo ya Walimu wangu, nashukuru niko vizuri kiafya. Mpira ni kazi yangu, lazima nijitume kama kawaida kwa lengo la kutimiza malengo yangu ambayo nimejiwekea kwa muda mrefu"
Wachezaji wa Yanga wanatarajiwa kurejea mazoezi siku ya kesho. Kabla ya kuanza mikikimikiki ya uwanjani wachezaji watafanyiwa vipimo vyote muhimu
Aidha uongozi wa Yanga utazungumza na wachezaji kuwakumbusha mikakati ya timu hiyo yenye lengo la kumaliza msimu kwa kishindo