Pamoja na uongozi wa Yanga kubainisha kuwa wameanza mchakato wa kuwarejesha makocha wao Luc Eymael (Kocha Mkuu) na Riedoh Berdien (Kocha wa viungo), Eymael amehofia huenda atachelewa kurejea nchini kutokana na kukumbana na changamoto ya usafiri huko Ubelgiji
Mbelgiji huyo ameeleza kufurahishwa na tamko la Rais Dk John Magufuli ambaye ametangaza shughuli zote za michezo kurejea kuanzia Juni Mosi
Hata hivyo amesema nchini kwao hakuna usafiri wowote wa Ndege utakaomuwezesha kuja Tanzania kabla ya Juni Mosi, hivyo huenda atalazimika kusubiri zaidi
Ni wazi, kama TFF itatangaza kuanza kwa ligi mwanzoni mwa mwezi Juni, huenda kocha msaidizi Charles Mkwasa atakabidhiwa majukumu ya kuwaongoza mabingwa hao wa kihistoria
Yanga inakabiliwa na michezo 11 ya kumalizia msimu lakini pia wana mechi ya robo fainali michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), droo yake ikitarajiwa kupangwa wakati wowote baada ya Rais Magufuli kuruhusu michezo
Yanga imepania kushinda ubingwa wa FA ili waweze kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao