Mshambuliaji wa Yanga Ditram Nchimbi amesema katika mambo ambayo hawezi kuyasahau tangu aliposajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria, ni kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambao Yanga ilifungwa mabao 3-0
Nchimbi anasema matokeo ya mchezo huo yalimvuruga sana hasa ikizingatiwa ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa nyota wengi wapya waliosajiliwa mwezi Januari akiwemo yeye mwenyewe
Lakini pia, ulikuwa mchezo wa kwanza kwa kocha Luc Eymael ambaye alitua kujiunga na mabingwa hao wa kihistoria mwezi huohuo
"Kwa kweli ule mchezo ulituumiza sana wachezaji pamoja na kocha (Eymael), ulikuwa ndio mchezo wetu wa kwanza. Wachezaji wengi wageni tulianza kuonekana pale baada ya kukosa michuano ya kombe la Mapinduzi," amesema
"Hata hivyo wakati mwingine inabidi kukubali, kuna wakati mpira unakuwa na matokeo ya kikatili sana, " aliongeza
Nchimbi amekuwa na mwanzo mzuri kwenye kikosi cha Yanga akiwa amefunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao
Jumla amefunga mabao matano kwenye ligi, matatu akiwa ameifunga Yanga wakati akiitumikia Polisi Tanzania
Ni miongoni mwa wachezaji ambao mashabiki wa Yanga wameweka matumaini makubwa kwao kuelekea msimu ujao
Uwezo wake wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji pamoja na winga, unampa nafasi zaidi ya kuendelea kutamba kwenye kikosi cha Eymael