Beki wa kulia wa Yanga Paulo Godfrey 'Boxer' amemtaja Mwinyi Zahera kocha wa zamani wa mabingwa hao wa kihistoria kuwa atabaki katika kumbukumbu zake
Zahera ndiye aliyempandisha Boxer kikosi cha kwanza cha Yanga kutoka timu ya vijana
Lakini pia, Mcongomani huyo alimbadilishia Boxer majukumu kutoka winga wa kulia na kuwa mlinzi namba mbili
"Nitamkumbuka sana Zahera, yule alikuwa ni zaidi ya kocha kwangu, kuna wakati alikuwa akifanya vitu kama mzazi," Boxer alinukuliwa na Mwanaspoti
"Nilikuwa na ndoto ya kuja kuitumikia Yanga kama winga au mshambuliaji lakini sio kuwa beki halafu watu wakanikubali. Zahera alinijenga sana na hata pale niliposema siwezi alinitia moyo"
"Nilitaka kupandwa na wazimu siku aliposema nitacheza mechi dhidi ya Simba. Kuna wachezaji wakubwa zaidi yangu huwa wanashindwa kumudu mchezo huu lakini Zahera aliniamini na baada ya mechi alinipongeza kuwa nimecheza vizuri"
Boxer amekaa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeraha ya nyama za paja aliyopata kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Township Rollers
Licha ya kupona majeraha hayo, bado hajafanikiwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kocha Luc Eymael akiahidi kuendelea kupambana ili kumshawishi Mbelgiji huyo