Baada ya Rais Dk John Magufuli kubainisha uwezekano wa ligi kuu kurejea, kocha mkuu wa Yanga Luc Eymael, amewaongezea program za mazoezi wachezaji wake ili kuhakikisha wanakuwa tayari pale itakapotangazwa tarehe ya kurejea dimbani
Katika program za mwanzo, wachezaji walikuwa wakipewa mazoezi ambayo walikuwa wakiyafanya mara moja tu asubuhi, lakini kwa sasa Eymael ameongeza program nyingine ya mazoezi ya jioni
Aidha Mbelgiji huyo aliyepania kumaliza kwa kishindo michezo iliyobaki, amewagawa wachezaji wake katika makundi ambapo kila kundi linafuatiliwa kwa ukaribu na mmoja wa makocha wake wa benchi la ufundi
Meneja wa Yanga Abeid Mziba amethibitisha kuwepo kwa utaratibu huo ambapo amesema mwanzoni walikuwa wakiwafuatilia wachezaji wote kwa pamoja
Apiga hesabu ya ubingwa wa FA
Kocha Eymael amepania kumaliza msimu na taji, baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu, hesabu zake amezielekeza zaidi kwenye michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC)
"Tumejiwekea malengo ya kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao, hivyo ni wazi tunapaswa kupambana ili tushinde ubingwa wa kombe la FA," alisema Eymael katika moja ya mahojiano yake
Yanga imetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la FA na ligi itakaporejea, droo ya hatua hiyo itafanyika
Timu nyingine zilizotinga robo fainali ni Simba, Azam, Alliance Fc, Ndanda Fc, Kagera Sugar, Sahare All Stars na Namungo Fc