Huko Uingereza, moja ya mapendekezo ambayo yametolewa na chama cha soka cha nchi hiyo wakati ligi itakaporejea, ni michezo iliyobaki kupigwa katika viwanja huru
Inaelezwa FA imependekeza viwanja 10 tu vitumike kumalizia mechi zote zilizobaki ambapo wamesema kama vilabu vitapinga pendekezo hilo basi watalazimika kufuta msimu
Kwa hapa Tanzania, siku chache zilizopita Bodi ya Ligi ilidokeza kuwa ligi inaweza kurejea mwezi ujao (kama Serikali itaruhusu) lakini hakutakuwa na mabadiliko ya utaratibu wa mechi kuchezwa
Kila timu italazimika kusafiri mikoani kwenda kucheza mechi zake zilizobaki kulinga na ratiba
Hata hivyo utaratibu huo huenda ukaviumiza zaidi vilabu wakati huu ambao tayari vina changamoto ya ukata baada ya ligi kusimama kwa karibu miezi miwili
Lakini pia mechi zilizobaki, zitachezwa bila ya mashabiki viwanjani pale Serikali itakapotoa ruhusa
Je vilabu vitawezaje kumudu gharama za kuwawezesha kufika katika mikoa ambayo watapaswa kucheza kama TFF haitatoa fungu lolote kusaidia?
Nakumbuka kocha mkuu wa Yanga Luc Eymael alipendekeza kuwa ni vyema TFF na Bodi ya Ligi ikafuata utaratibu ambao Uingereza wanataka kutumia kwa kuweka vituo ambavyo vitatumika kukamilisha mechi zilizobaki
Eymael alipendekeza mechi hizo zipigwe jijini Dar es salaam, timu ziweke kambi katika maeneo ambayo itakuwa rahisi kusimamia wachezaji na wahusika wa timu
Lakini ni wazi kama Bodi ya Ligi itasisitiza timu kusafiri mikoani kucheza mechi zao wakati huu ambao haziingizi fedha, haitashangaza kuona timu nyingi zikishindwa kufika vituoni