Yanga imedhamiria kuimarisha kikosi chake hasa safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na kikosi bora ambacho kitaweza kushindania ubingwa wa ligi kuu
Jambo la uhakika ni kuwa kuna michakato mingi ya usajili mabingwa hao wa kihistoria wanaiendesha chini kwa chini na pengine itawekwa hadharani pale dirisha la usajili litakapofunguliwa
Baada ya mkataba wake na Rayon Sports kuvunjwa, mshambuliaji Michael Sarpong raia wa Ghana amekuwa miongoni mwa nyota wanaotajwa kuwaniwa na mabingwa hao wa kihistoria
Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ameeleza kuvutiwa na mshambuliaji huyo na kutamani kufanya nae kazi msimu ujao
Akiwa na Rayon Sports, kwenye msimu wake wa kwanza, Sarpong mwenye umri wa miaka 23 aliifunga mabao 16 na kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Rwanda
Mkataba wake ulivunjwa mwezi uliopita baada ya kudaiwa kutoa maneno ambayo yalionekana kuwa ni dharau kwa mabosi wa klabu yake
"Ni mshambuliaji mzuri na ningependa kufanya nae kazi msimu ujao na katika mashindano ya Kimataifa kama tutapata nafasi," Eymael amenukuliwa na Mwananchi
"Sarpong ni mpambanaji akiwa uwanjani na muda wote ni mwenye uchu wa kufunga, anajua kujiweka katika nafasi ya kufunga"
"Naamini uwezo wake kwa kushirikiana na wachezaji tulionao sasa atafanya vizuri. Bado tunaimarisha kikosi chetu tunataka kuwa na wachezaji bora"