Baada ya jitihada za kumpata kocha wa Kagera Sugar Meckie Mexime kugonga mwamba, uongozi wa Yanga huenda ukamgeukia kocha mkuu wa Namungo Fc Hitimana Thiery
Yanga imedhamiria kuuanza msimu ujao ikiwa na kocha msaidizi ambaye atafanya kazi na Luc Eymael wakati Charles Mkwasa akitarajiwa kupandishwa cheo kuwa Mkurugenzi wa Ufundi
Inaelezwa Hitimana ambaye ameifanya Namungo Fc kuwa moja ya timu tishio kwenye ligi kuu msimu huu ikiwa inashika nafasi ya nne, jina lake tayari liko mezani kwa wadhamini wa Yanga kampuni ya GSM
"Mpango wa kumpata Mexime umeshindikana baada ya viongozi wa Kagera kuamua kupandisha dau na kumbakiza hivyo jina la Hitimana limeshapelekwa kwa GSM ambao watakamilisha suala lake.
"Yanga inahitaji kuboresha bechi la ufundi anahitajika kocha atakayeongeza nguvu lakini pia watu wenye sifa za kukaa eneo hili litawagusa meneja, watunza vifaa na daktari wawe na vigezo," alisema mtoa taarifa
Mwenyewe Hitimana amesema hana tatizo kufanya kama atapata nafasi ya kufanya kazi Yanga kwani kilichomleta nchini ni kufanya kazi
"Nimekuja Tanzania kufanya kazi nipo tayari kwenda timu yoyote, suala la mkataba wangu na Namungo unamalizika mwezi huu, lakini nitakuwa na timu hiyo hadi ligi itakapomalika baada ya hapo nitaamua kama kuendelea kufanya kazi nao au kuangalia sehemu nyingine," alisema