Ifikapo kesho Jumanne, May 05 uongozi wa Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla utatimiza mwaka mmoja tangu walipoingia madarakani mwaka uliopita
Kwa kiasi kikubwa Dk Msolla amefanikiwa kufanya kile alichoahidi kwenye kampeni za uchaguzi mwaka jana
Ndani ya mwaka mmoja tumeshuhudia Yanga ikifanya jitihada za kujikwamua kutoka utegemezi na kuwa klabu inayojitegemea
Kama sio janga la corona, pengine leo Yanga ingekuwa tayari imeingia kwenye mfumo mpya wa uendeshaji
Ni ahadi ambayo Dk Msolla aliitoa akiahidi kubadili mfumo wa uendeshaji ndani ya miezi 12
Zipo changangoto ambazo zilimpa wakati mgumu hasa pale wachezaji walipovunja mikataba kutokana na suala la kukosa mishahara
Lakini juhudi walizionyesha na hata ujio wa GSM ni miongoni mwa jitihada ambazo uongozi wake umefanya kwa kushirikiana na wadau wengine wa Yanga hapa tunaweza kumtaja Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde ambaye aliongoza kamati ya Hamasa na Michango
Mavunde amekuwa mstari wa mbele kutoa maoni, mapendekezo na ushauri ili kuweka mambo sawa pale zinapotokea changamoto
Yanga imetoka kwenye kipindi kigumu sana lakini mwanga wa 'neema' tayari umeanza kuonekana
Muhimu ni kwa Wanayanga kuendelea kuwa pamoja ili kuhakikisha timu inafikia malengo yake