Afisa Mhamasishaji wa klabu ya Yanga Antonio Nugaz amesisitiza kuwa klabu ya Yanga ingependa kuona bingwa wa ligi kuu anapatikana uwanjani na sio kwa kutumia vigezo ambavyo havipo
Akihojiwa na Azam TV jana, Nugaz alisema TFF haina kanuni ya dharura inayoelekeza ni utaratibu gani unapaswa kuchukuliwa pale ligi inaposhindikana kumalizika tofauti na nchi nyingine kama Kenya ambao wametumia kanuni yao ya dharura kuipa ubingwa Gor Mahia
Amesema kama TFF italazimika kutumia matokeo ya msimu huu, Yanga ina mchezo mmoja wa kiporo hivyo ni lazime wacheze ili kuweka usawa na timu nyingine
Aidha kwa upande wa Wawakilishi wa michuano ya CAF msimu ujao, Nugaz amesema kama CAF watafuta michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu basi TFF wanaweza kufuta ligi na msimu ujao wawakilishi wa msimu uliopita (Simba, Yanga, Azam Fc na KMC) wakaenda kushiriki
Lakini kama CAF watafuta michuano hiyo kuanzia hatua ya makundi ni wazi Tanzania itakuwa imepoteza nafasi zake nne kwa Libya hivyo msimu ujao watakuwa na wawakilishi wawili
Hapo amependekeza TFF iangalie timu zenye alama nyingi kwenye ushiriki wa michuano ya CAF (Ligi ya mabingwa na kombe la Shirikisho) kuzipatia tiketi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao
"Kwa mazingira haya sisi tungependa zaidi ligi imalizike ili kila timu ipate haki yake inayostahili," alisema
Hivi karibuni Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) lilitoa waraka kwa wanachama wake kuweka wazi hatma za ligi zao msimu huu kutokana na janga la corona
CAF ilitoa siku saba kwa nchi Wanachama kuweka hadharani misimamo yao
Nchi za Guinea, Kenya na Angola tayari zimetangaza kufuta misimu yao ambapo kwa Kenya, FKF ilitumia kanuni ya dharura kuipa ubingwa Gor Mahia
Kanuni hiyo inaelekeza kama ligi haitamalizika kutokana na sababu yoyote, na ikiwa zaidi ya nusu ya mechi zimeshachezwa, msimamo wa nusu ya msimu utatumika kama msimamo wa mwisho
Guinea na Angola zimefuta misimu pasi na kuwa na bingwa kwa kuwa nazo hazina kanuni za dharura