Mshambuliaji wa zamani wa Yanga Amissi Tambwe raia wa Burundi, amesema hana mpango wa kustaafu kucheza soka miaka ya karibuni kwani bado anao uwezo wa kutupia mabao
Tambwe mwenye umri wa miaka 31, amesema ana angalau misimu minne ya kucheza soka la ushindani kabla ya kufikiria kustaafu
"Nina umri wa miaka 31, nitaendelea kucheza soka la ushindani kwa misimu minne au zaidi kabla ya kufikiria kustaafu," amesema
"Mimi ni mchezaji ninayejiheshimu, najitunza, naishi kwa kufuata misingi yote ambayo mchezaji wa mpira wa miguu anapaswa kuishi"
"Sinywi pombe, sivuti sigara, nina mke na sijawahi kufikiria kwenda kujirusha kumbi za starehe. Mawazo yangu yote yako kwenye soka"
Tambwe ameacha historia ya kuvutia kunako klabu ya Yanga aliyoitumikia kwa misimu minne na kushiriki kutwaa ubingwa wa ligi kuu misimu mitatu mfululizo
Aidha amepongeza mchakato wa mabadiliko unaofanywa na Yanga sasa akiamini kuanzia msimu ujao, mabingwa hao wa kihistoria watakuwa na timu yenye ushindani sawa au zaidi ya wapinzani wao Simba ambao kwa miaka ya karibuni wamefanikiwa kutokana na uwezo wa kifedha uliowafanya waweze kusajili wachezaji wazuri
"Nimefurahi kusikia Yanga wameanza mchakato wa mabadiliko, hilo ni jambo zuri sana kwa sababu sasa watakuwa na uwezo wa kununua wachezaji wote wanaowataka kutokana na uwezo wa kifedha watakaokuwa nao"
Tambwe amesema msimu ujao atarejea kwenye soka la ushindani akifichua kuwa kama mambo yakienda sawa, anaweza kurejea hapa Tanzania kuendea na maisha yake ya soka
Baada ya kuachwa na Yanga, Tambwe alielekea Oman ambako alijiunga na Fanja Fc. Hata hivyo alivunja mkataba wake miezi michache baadae kutokana na matatizo ya kifamilia