Said Mwamba 'Kizota', jembe la Yanga lililocheza Simba bila kutarajia

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
1 May 2020
Said Mwamba 'Kizota', jembe la Yanga lililocheza Simba bila kutarajia

Nchini Tanzania ni vilabu vya Yanga na Simba pekee ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka 80

Vilabu hivi vimekuwa na utamaduni ambavyo unavifanya kuwa tofauti sana. Hakuna urafiki pamoja na kuwa mashabiki zake ni marafiki na ndugu kabisa

Kwa wachezaji, unapocheza moja ya klabu hizi, unakuwa na heshima kubwa mtaani

Ikitokea umehama kutoka klabu moja kwenda nyingine, kwa mashabiki hilo ni kosa kubwa sana ambalo wengine hawawezi kukusamehe

Lakini pamoja na madhira yake, utamaduni wa wachezaji kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine umekuwepo toka zamani

Tena miaka ya zamani lilikuwa jambo gumu sana kukubalika, wachezaji waliohama kutoka upande mmoja kwenda mwingine, wakati mwingine waliingia matatani

Miongoni mwa wachezaji ambao wamezitumikia timu zote (Yanga na Simba) ni marehemu Said Mwamba 'Kizota' aliyefariki dunia mwaka 2007 kwa ajali ya kugongwa na gari

Kama yupo mchezaji ambaye aliwapa raha mashabiki wa timu zote hizo, basi ni Kizota aliyefariki dunia Februari 11, mwaka 2007.

Kizota ni mchezaji aliyewasisimua kwa namna yake mashabiki wa Yanga na Simba kutokana na mabao yake.

Umauti ulimfika wakati akiwa anatoka kushuhudia mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, Raundi ya Awali kati ya wenyeji Simba dhidi ya Textil de Pungue ya Msumbiji.

Kama kuna miaka ambayo Kizota alifanya vitu vya ‘babu kubwa’ kwenye soka ya Tanzania, basi ni 1993, kwani mapema tu mwaka huo aliibuka mfungaji bora kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda, akiiwezesha Yanga pia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwafunga wenyeji, SC Villa.

Lakini pia, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Tanzania. Yote tisa, kumi ni pale Kizota alipofunga mabao mawili peke yake, wakati Yanga inaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam.

Ilikuwa ni Machi 27, mwaka huo 1993, wakati Kizota alipomchambua kipa hodari nchini enzi hizo, Mwameja Mohamed katika dakika za 47 na 57. Simba ikielekea kulala 2-0, shukrani kwake Edward Chumila (naye marehemu pia) aliyewafungia Wekundu wa Msimbazi bao la kufutia machozi, dakika ya 75.

Baada ya kipigo kikali cha mabao 4-1, Julai 2, mwaka 1994, Yanga ilivunja kikosi ikiwafukuza karibu nyota wake wote wa kikosi cha kwanza kwa tuhuma za kuhusika kuihujumu timu katika kipigo hicho kilichotokana na mabao ya George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani na Dua Saidi, bao la kufutia machozi la Yanga likifungwa na beki imara, Constantine Kimanda.

Kati ya nyota waliotupiwa virago Yanga ni Kizota, ambaye kutokana na makali yake wakati huo, akiwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania na miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa kwenye kikosi kilichochukua Kombe la Challenge nchini Kenya, Simba wakamsajili

Kizota alitaka kuwaonyesha Yanga kwamba, walifanya kosa kumwacha na katika mchezo wa marudiano baina ya watani hao wa jadi wa Ligi Kuu ya Bara, Oktoba 4, 1995, Yanga ikiwa inaelekea kabisa kushinda mchezo huo 1-0, Said Mwamba alitibua furaha ya wana Jangwani dakika ya 70 kwa kufunga bao safi la kusawazisha.

Yanga ilitangulia kupata bao kupitia kwa mpachika mabao wake mahiri enzi hizo, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ dakika ya 40. Bao la Kizota liliwachanganya Yanga na dakika tisa baadaye, wakapachikwa bao la pili. Safari hiyo alikuwa ni Mchunga Bakari ‘Mandela’ aliyewaambia wana Jangwani; kutangulia si kufika.

Baada ya msimu huo, Yanga walikiri kosa lao na wakaenda kumpigia magoti Kizota arejee nyumbani. Kwa sababu Kizota alikuwa anaishi nyumba ya pili kutoka klabu ya Yanga, akiishi na mkewe Tosha, Mtaa wa Jangwani, hivyo ilikuwa rahisi kumrejesha nyumbani.

Na aliporejea Yanga, Kizota aliifunga tena Simba. Ilikuwa Novemba 9, mwaka 1996, katika sare ya ajabu ya watani, ya mabao 4-4 mjini Arusha.

Kizota aliifungia Yanga bao la kusawazisha lililofanya sare ya 3-3 katika dakika 70, baada ya awali Kipese kuifungia Simba, dakika ya saba, Edibily Lunyamila kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 28, Ahmed Mwinyimkuu kuifungia Simba la pili dakika ya 43, kabla ya Dua Said kufunga la tatu dakika ya 60 na Mustafa Hoza kuisawazishia Yanga kwa kujifunga dakika ya 64.

Sanifu Lazaro aliifungia Yanga bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 75, lakini walishindwa kulinda lango lao na kuruhusu bao la dakika za lala salama, lililofungwa na Duwa Said dakika ya 90, hivyo kuwa sare ya 4-4.

Kizota alijiunga na Yanga mwaka mwaka 1988, akitokea timu ya Shirika la Posta la Tabora, enzi hizo likijulikana kama Posta na Simu, wakati akicheza kama kiungo.

Baada ya kung’ara akiwa na Yanga, msimu wa 1988 ulipomalizika alichukuliwa na Al-Jazira ya Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.

Akiwa Abu Dhabi katika timu yake mpya, Kizota alikutana na aliyekuwa nyota wa timu ya Taifa ya Malawi, Lawrence Waya, ambaye alikuwa winga machachari sana enzi zake.

Kwa pamoja Kizota na Waya waliifanya timu yao kuwika mno katika soka ya Uarabuni.

Kutokana na vitu vyake vya uhakika, Kizota alikubalika mno na mashabiki wa soka Abu Dhabi, jambo ambalo lilifanya Waarabu waanze kumrubuni abadili uraia na kuwa raia wa huko.

Ghiliba hizo hakupewa Kizota peke yake, bali hata Waya. Kizota aliingiwa na ghiliba hizo na kuanza kufanyiwa taratibu za kupewa uraia, lakini wakati taratibu zikifanywa, mwanasoka huyo aliomba likizo ya kurejea nyumbani Tanzania kuoanana na familia yake na ndipo alipobadili mawazo ya Uarabu.

Hiyo ilikuwa ni mwaka 1989. “Hakuna kingine ni Yanga tu, nilipofika tu viongozi wakasema wananihitaji sana, hivyo nikaamua kubaki Yanga,” alisema Kizota kwenye moja ya mahojiano yake mwaka 1999.

Kizota aliingia kwa makeke, safari hiyo hakuwa kiungo, bali alihamia kwenye nafasi ya ushambuliaji na kufanikiwa kuipeleka Yanga kileleni kwa mabao yake.

hata hivyo, viongozi wa timu yake baada ya kuona kimya kimezidi, walimtaka haraka sana kurejea. Alitumiwa ujumbe wa simu ya maandishi (Fax) ambao aliupuuza, lakini baadaye alifuatwa na viongozi hao walioondoka naye kurejea Abu Dhabi.

Kizota aliondoka nchini akiwa anaongoza kufunga mabao na Ligi imefikia ukingoni, huku Yanga ikihitaji pointi chache tu kutangaza ubingwa, jambo ambalo liliwezekana, licha ya yeye kuondoka na vijana wa Jangwani kurejesha taji walilopokonywa na Coastal Union ya Tanga mwaka 1988.

Kizota aliishi Uarabuni hadi mwaka 1991, aliporejea kupumzika na kuikuta Yanga ikiwa katika hali mbaya, soka ya Tanzania inatawaliwa na watani wao wa jadi, Simba, ambayo mwaka huo wakati anarejea (Simba) ilikuwa imetangaza ufalme wa soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame.

"Kama nilivyokwambia naipenda sana Yanga, nikaamua kubaki, lakini jamaa (Al-Jazira) walikuwa wakinitaka nirejee haraka sana, nikawadanganya naumwa, wakati wananitumia fedha za matibabu, kumbe mie niko safi kabisa", maneno ya marehemu Kizota, aliyehitumu elimu yake ya msingi mwaka 1981 katika shule ya Mabatini, Tabora alikozaliwa.

Kizota aling’ara Yanga tangu mwaka huo, akiiwezesha kutwaa Kombe la Kagame mwaka 1993, kufika fainali ya michuano hiyo mwaka 1992, Nusu Fainali nchini Sudan mwaka 1994, kabla ya 1994 kuhamia Simba.

Aliporejea Yanga 1996, alicheza kwa misimu miwili zaidi kabla ya mwaka 1998 kutimkia Al-Nasar ya Oman. Alikaa huko msimu mmoja tu, kabla ya kurejea nchini katikati ya msimu wa Ligi Kuu na kujiunga na timu iliyokuwa Daraja la Kwanza, Kariakoo United ya Lindi, ambako akiwa na wakongwe wenzake kama Mustafa Hoza waliipandisha Ligi Kuu.

Baada ya kuipandisha timu hiyo, Kizota alirejea Yanga ambako aliiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame tena Uganda mwaka 1999, ingawa kutokana na umri wakati huo, alirejea kucheza nafasi ya ulinzi. Hadi anafariki dunia, Kizota alikuwa mume wa Tosha na baba wa watoto wawili, Hamim na Rabii

Mwenye ez Mungu ampe pumziko la Milele mwamba huyu aliyeacha historia ya kipekee ndani ya klabu ya Yanga

ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
1h ago
READ MORE β†’
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
2h ago
READ MORE β†’
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
5h ago
READ MORE β†’
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
9h ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
12h ago
READ MORE β†’
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
13h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
16h ago
READ MORE β†’
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
1d ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
1d ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
1d ago
READ MORE β†’