Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ameunga mkono msimamo wa mabosi wake juu ya hatma ya ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom msimu huu akitaka TFF isubiri wakati mwafaka kuruhusu mechi zilizobaki zichezwe ili bingwa apatikane uwanjani
Barani Ulaya nchi za Uholanzi, Ubelgiji na Ufaransa zimetangaza kumaliza msimu bila kuchezwa mechi zilizosalia baada ya Serikali za nchi hizo kutangaza kutoruhusu ligi hizo kurejea kabla ya mwezi Septemba
Nchini Ufaransa klabu ya PSG inatarajiwa kutangazwa kuwa mabingwa ambapo imeelezwa msimamo wa ligi wa sasa utatumika
Hatua kama hizo zimechukuliwa na Shirikisho la soka la Kenya (FKF) kwa kumaliza msimu bila ya raundi 11 zilizobaki kuchezwa na wakati huohuo wakiitangaza Gor Mahia kuwa mabingwa kwa kutumia msimamo wa sasa wa ligi hiyo licha ya uamuzi huo kusababisha mvutano kati ya Bodi ya Ligi ya Kenya na FKF
Kwa mtazamo wake, Eymael amesema upo uwezekano wa mechi zilizobaki kuchezwa kwani ni chache, hakuna haja ya kuchukua uamuzi wa jumla kama zilivyofanya baadhi ya nchi
Eymael amesema amezungumza na Mwenyekiti wa Yanga, Dkt Mshindo Msolla ili akawasilishe maoni na mapendekezo yake kwa viongozi wa TFF ili wasifute ligi hiyo na wajaribu kuwa na subira.
"Nimemuambia Mwenyekiti wa Yanga (Dk Msolla) akaongee na TFF, na kuwashahuri wasifute ligi na kwamba wachukue hatua kama michezo ifanyike kwenye viwanja vya Dar es Salaam tu ili kurahisisha umalizikaji wake," amesema
"Kabla ya mechi kuchezwa, wachezaji wote wapimwe virusi vya corona ili kuepuka maambukizi mapya kwa wachezaji na viongozi watakaoruhusiwa kuingia uwanjani wakati wa mechi hizo, ambazo hazitakuwa na watazamaji"
Uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya ligi kuu utatolewa na TFF ambayo hata hivyo inasubiri mwongozo wa Serikali juu ya nini kifanyike
Hata hivyo kama ligi itashindwa kurejea mwezi May, upo uwezekano mkubwa itamalizwa bila ya mechi zilizosalia kuchezwa