Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ameeleza kuridhishwa kwa asilimia 90 na mazoezi binafsi yanayofanywa na wachezaji wake wakati huu ambao ligi imesimama kutokana na janga la corona
Kama zilivyo timu nyingi, benchi la ufundi la Yanga liliwapa wachezaji program maalum za mazoezi ambayo wanapaswa kuyafanya majumbani kwao ili kulinda viwango vyao
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema Eymael ameridhishwa na kile kinachofanywa na wachezaji wake
"Kocha ameeleza kuridhishwa na mwenendo wa mazoezi wanayofanya wachezaji ambayo aliwaachia kabla hajaondoka kwenda Ubelgiji," amesema
"Ametuma program nyingine ambayo tulimkabidhi nahodha Papy Tshishimbi ahakikishe inawafikia wachezaji wote"
"Kocha wetu wa viungo nae amekuwa akifuatilia mazoezi hayo ambapo wachezaji wanamtumia vipande vya video. Kila kitu kiko sawa, nadhani hatutakuwa na changamoto kubwa pale ligi itakaporejea"
Yanga yenye alama 51 ikiwa inashika nafasi ya tatu, ina mechi 11 za kumalizia pamoja na kusubiri droo ya kombe la FA (ASFC) hatua ya robo fainali