Hivi karibuni kuliibuka taarifa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael alipendekeza kusajiliwa kwa kiungo mkabaji ambaye atawapa changamoto viungo waliopo
Baadae ikaelezwa kuwa Yanga inakaribia kumnasa nyota wa Rayon Sports Ally Niyonzima ambaye ni kiungo mkabaji anayecheza timu Taifa ya Rwanda pia
Taarifa hizo zimemfikia nahodha wa Yanga Papy Tshishimbi ambaye amebainisha kuwa yuko tayari kwa changamoto
Tshishimbi amesema yeye ni mchezaji anayependa kupata changamoto kwenye kila jambo analofanya kwani anaamini kupitia changamoto hiyo itamfanya kuwa bora zaidi
"Nimefurahi kusikia hivyo na niko tayari kwa changamoto mpya. Unajua kunapokuwa na ushindani wa namba humfanya mchezaji ajitume na mwisho wa siku timu na mchezaji mwenyewe atanufaika. Hivyo mimi namkaribisha mchezaji yeyote atakayesajiliwa ili tuweze kupambana kuifanya Yanga iwe bora zaidi," amesema
Tangu awasili kocha Luc Eymael, Tshishimbi amekuwa mchezaji tegemeo nafasi ya kiungo mkabaji na pale alipokosekana uwanjani, timu ilionekana kupoteza mwelekeo