Mshambuliaji wa Difaa El Jadid Simon Msuva amesema kiungo Haruna Niyonzima, amechangia kwa kiasi kikubwa kumuimarisha wakati akiitumikia Yanga
Msuva amebaki nchini Morocco baada ya ligi ya nchi hiyo kusimama kutokana na corona, amesema Niyonzima alikuwa mstari wa mbele kumpa moyo na kumsukuma afanye vizuri pale aliposhindwa
Msuva amemtaja Niyonzima kama mchezaji wake bora wa muda wote aliyewahi kucheza nae hapa Tanzania
"Haruna Niyonzima ndio mchezaji bora wa kigeni kwangu ambaye nilichezanaye timu moja (Yanga) wakati nacheza Tanzania. Tukiwa uwanjani kila nilipokosea alikuwa ananiita na kuniambia nini cha kufanya. Haruna ni mtu ambaye amenisaidia sana hata nje ya uwanja," amesema
"Wakati nazomewa na mashabiki wa Yanga Niyonzima alikuwa ananipa sana moyo, alikuwa ananiambia nisiweke akilini maneno ya mashabiki nachotakiwa ni kucheza mpira na kufanya kile ninachoona ni sahihi"
"Alikuwa msaada mkubwa kwangu japokuwa wachezaji wengine walikuwa wananishauri ila yeye alikuwa mbele sana. Atabaki kuwa mchezaji bora sana kwangu na uwanjani hakuna asiyemjua Niyonzima"
Msuva anapeperusha vyema bendera ya Tanzania huko Morocco akiwa mmoja wa wachezaji wanaofanya vuzuri kwenye ligi ya nchi hiyo