Beki kiraka wa Yanga Ally Mtoni 'Sonso' amesema hawezi kumsahau aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Emmanuel Amunike kwa kuwa alikuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha kiwango chake
Amunike alimjumuisha Sonso kwenye kikosi cha Stars kilichoshiriki michuano ya Afcon 2019 nchini Misri
Nyota huyo aliyetua Yanga akitokea klabu ya Lipuli FC, alikuwa sehemu ya kikosi kilichokata tiketi ya michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya kufuzu mara ya kwanza mwaka 1980
"Nilisikitika sana pale Emmanuel Amunike alipoondolewa katika Timu ya Taifa (Taifa Stars). Amunike ni kocha ambaye aliniita kwenye timu ya Taifa kwa mara ya kwanza, na alinijumuisha kwenye kikosi kilichoenda Misri kucheza AFCON. Ni kocha mwenye mchango mkubwa kwangu, kwani kuniita timu ya Taifa kuliniimarisha kisoka," Sonso aliiambia eFM
Beki huyo anayeweza kucheza nafasi zote za ulinzi pamoja na kiungo mkabaji, amesema wakati huu ambao ligi imesimama anafanya mazoezi binafsi kuhakikisha anakuwa fiti pale ligi itakaporejea
Tangu ajiunge na Yanga, Sonso amekuwa na msimu mzuri kwani anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara pamoja na ushindani uliopo kwenye safu ya ulinzi
Amkubali Makambo
Katika hatua nyingine, Mtoni amesema Heritier Makambo ni mmoja wa washambuliaji ambao alikuwa na wakati mgumu kukabiliana nao wakati akiwa klabu ya Lipuli
Mtoni amesema Makambo pamoja na Meddie Kagere wa Simba, ndio washambuliaji anaowakubali zaidi miongoni mwa washambuliaji aliowahi kukabiliana nao

Huenda msimu ujao Mtoni akacheza pamoja na Makambo kwani Yanga imedhamiria kumrejesha kundini mbabe huyo wa kuzifumania nyavu ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Horoya AC