Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Alsmas Kasongo amesema kwa sasa ni mapema mno kufikiria kumaliza msimu kutokana na janga la corona, lakini pia maamuzi yoyote yatatolewa na kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF)
Hivi karibuni kumeibuka mjadala baada ya baadhi ya wadau kupendekeza ligi imalizwe na klabu ya Simba inayoongoza ligi hiyo kupewa ubingwa
Jana Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli alisema msimamo wa klabu hiyo ni kuona mechi zilizobaki zinachezwa pale changamoto ya corona itakapomalizika ili bingwa apatikane uwanjani
Bumbuli alisema kimahesabu, Yanga inaweza kufikisha alama 84 kama itashinda mechi zake zote zilizobaki hivyo wanaweza kushinda ubingwa kama ikitokea timu nyingine hazitafikisha idadi hiyo ya alama
Kasongo, Bosi wa Bodi ya Ligi amesema hakuna kanuni yoyote inayoelekeza hatua za kuchukuliwa pale ligi inaposhindikana kufika mwisho hivyo uamuzi wowote utaamuliwa na kikao cha Kamati ya Utendaji kwa kuwashirikisha wadau
Aidha Kasongo amesema ni wakati TFF na wadau wake kukaa chini kutengeneza kanuni ambayo itaepusha sintofahamu juu ya hatua za kuchukuliwa pale ligi inapokwama
"Kanuni hazisemi linapotokea janga kama hili nini kifanyike, zinazungumzia tu mchezo. Pengine ni wakati mwafaka kufanya maboresho ya kanuni baada ya janga hili," amesema
Hata hivyo Rais wa TFF Wallace Karia amesema kwa sasa hakuna hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa hadi hapo Serikali itakapotaoa mwongozo wake
Kumekuwa na makundi tofauti miongoni mwa wadau wanaopendekeza nini kifanyike kama ikitokea ligi haitawezekana kumalizika
Kundi la kwanza ni wale wanaotaka timu inayoongoza ligi ipewe ubingwa kisha kuwe na mechi chache za 'play-off' kusaka nafasi ya pili na timu za kushuka daraja
Kundi jingine linataka subira iendelee kutawala ili mambo yatakapotulia basi ligi iweze kuendelea. Hata hivyo changamoto hapa ni muda kwani inawezekana jambo hilo likachukua muda mrefu pengine hata kuathiri muda wa kuanza msimu ujao
Lakini pia wapo wanaopendekeza mechi za playoff zichezwe kutafuta bingwa wa ligi kuu na timu zinazopaswa kushuka daraja huku kundi jingine likipendekeza msimu mzima ufutwe kama ilivyofanya nchi ya Uholanzi
Uamuzi huo pia uhusishe ligi daraja la kwanza, la pili na madaraja mengine ili msimu ujao timu zote zianze upya