Uongozi wa klabu ya Yanga umekiri kuwepo kwa madeni ya baadhi ya makocha, wachezaji waliopita klabu hiyo miaka ya nyuma
Hivi karibuni kuliibuka taarifa kuwa mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Obrey Chirwa alipeleka malalamiko FIFA akiataka kulipwa fedha anazoidai Yanga ambazo zinafikia Tsh Milioni 40
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema ni kweli madeni hayo yapo, uongozi wa sasa uliyakuta na wanawajibika kuyalipa
Hata hivyo amesema wanachokifanya sasa ni kuhakiki madeni hayo kabla ya kuanza kulipa
"Ni kweli kuna wachezaji wana madai ya fedha za ada ya usajili miaka ya nyuma na kuna wengine wanadai baadhi ya mishahara yao ya zamani. Kinachofanyika sasa ni kuhakiki taarifa za madeni yote kabla ya kuanza kuyalipa kama inavyotakiwa," amesema Bumbuli
Wachezaji wanaotajwa kuidai Yanga ni pamoja na Youthe Rostand, Haji Mwinyi, Chirwa, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe na Donald Ngoma wakati kwa upande wa makocha wamo Mwinyi Zahera, Hans van Pluijm na George Lwandamina aliyerejea klabu ya Zesco United
Madeni hayo yalilimbikizwa kipindi Yanga ilipokumbwa na ukata baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wake na Mdhamini Mkuu, Yusufu Manji kujiondoa Yanga
Hivi karibuni Bodi ya ligi ilitangaza kuwa kuanzia msimu ujao timu ambazo zinadaiwa na wachezaji hazitaruhusiwa kushiriki ligi kuu