Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael amekwama huko Ubelgiji kutokana na janga la corona
Kumekuwa na uhaba wa Ndege kutoka barani Ulaya kuja Afrika baada ya mataifa mengi kusitisha huduma hiyo kutokana na janga la corona
Lakini pia kwa hapa Tanzania, Serikali imesitisha safari za ndege za abiria za Kimataifa kwa muda wakati ikiendelea na jitihada za udhibiti wa ugonjwa wa corona
Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amesema Eymael amebuni utaratibu wa kuwasiliana na wachezaji wake kuwapa maelekezo ya mazoezi ambayo wanapaswa kufanya
Nugaz amesema Eymael amekuwa akiwasiliana na wachezaji moja kwa moja kupitia WhatsApp kuwapa maelekezo pamoja na kupata mrejesho wa kila wachoelekezwa kufanya
"Mwalimu bado ameshindwa kurejea nchini kutokana na janga hili la corona ambalo ni tishio kwa dunia nzima. Lakini amekuwa akitoa program na maelekezo kwa wachezaji kupitia WhatsApp, Tunafurahi wachezaji wanayafuata maelekezo hayo," amesema
Hivi karibuni Eymael alisema anafanya jitihada ili aweze kurejea nchini haraka kwani kukosekana kwake kunasababisha mambo mengi kutokwenda sawa
Hata hivyo kwa sasa hana la kufanya kwa kuwa suala la kulinda afya na uhai kutokana na tishio la corona ni muhimu zaidi