Bado janga la corona limezuia kurejea kwa mikikimikiki ya ligi kuu ya Vodacom pamoja na ligi mbalimbali kote duniani
Benchi la ufundi la Yanga kama ilivyokuwa kwa timu nyingi, lilitoa program ya mazoezi kwa kila mchezaji ambayo alipaswa kwenda kufanya nyumbani
Meneja wa Yanga Abeid Mziba amefichua kuwa pamoja na wachezaji kupewa program hiyo, waliandaa utaratibu wa kuwafuatilia kila mchezaji kuhakikisha wanatekeleza program hiyo
Mziba ameeleza kuridhishwa na mwenendo wa wachezaji na ana imani ligi itakaporejea kocha Luc Eymael hatakuwa na kazi kubwa ya kufanya
"Nimekuwa nikimfuatilia kila mchezaji katika mazoezi yao, wana morali ya kutosha na mazoezi yanaridhisha hivyo kocha hatakuwa na kazi ngumu," amesema Mziba
Eymael alipaswa kurejea nchini keshokutwa Jumatano lakini alilazimika kufuta safari yake baada ya Serikali ya Tanzania kusitisha safari zote za ndege kutoka nje ya nchi
Mbelgiji huyo huenda akalazimika kusubiri mpaka pale mambo yatakapokuwa sawa
Hata hivyo hakuna uwezekano wa ligi kuendelea siku za karibuni kutokana na mwenendo wa maambukizi ya virusi vya corona nchini