Inaelezwa miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na kocha Luc Eymael katika maboresho ya kikosi chake, ni pamoja na kuongezewa mlinda lango mkali zaidi ya waliopo
Kwa sasa Yanga inawategemea zaidi Metacha Mnata na Farouk Shikhalo huku Ramadhani Kabwili akishindwa kupenya kwenye kikosi cha kwanza
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amefichua kuwa Eymael ametaka aletewe mlinda lango ambaye atawapa changamoto makipa hao wa timu za Taifa za Tanzania na Kenya
Pamoja na mpango wa kusajili nyota wapya wanne wa kigeni ambao ni beki, kiungo, winga na mshambuliaji, nafasi nyingine ambazo zitaongezewa nguvu ni beki wa kulia na kushoto na golikipa

"Ripoti ya kocha imeweka wazi kitu gani kinatakiwa kufanyika, anahitaji kipa, mabeki watatu, kiungo na mshambuliaji, lengo kubwa ni kuimarisha safu ya ulinzi na ushambuliaji"
"Kuhusu kuanza usajili kamati husika zinaendelea na mchakato, nawaambia tu Wanayanga kuwa wawe watulivu, usajili utafanyika mzuri na watafurahi wenyewe," alisema Mwakalebela
Yanga kupitia wadhamini/wahisani GSM, wameanza michakato ya usajili mapema kwa kuhuisha mikataba ya wachezaji ambayo inaelekea ukingoni
Muhimu zaidi wamefanikiwa kuwazidi ujanja watani zao Simba waliokuwa wamejitosa kuwawania nyota wao muhimu Bernard Morrison na Papy Tshishimbi baada ya kufanikiwa kuwaongezea mikataba