Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema timu yao imejipanga kupambana kuhakikisha wanamaliza msimu wakiwa katika nafasi nzuri
Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama 51 baada ya kushuka dimbani mara 27, wako nyuma kwa alama 20 dhidi ya vinara wa ligi hiyo, Simba
Wamesalia na mechi 11 ambazo hata hivyo zinawapa nafasi finyu ya kutwaa ubingwa msimu huu
Mwakalebela amesema kwa sasa wanasikiliza mamlaka ya Serikali na zile za usimamizi wa soka nchini, Afrika na Duniani kwa ujumla wakati huu wa janga la Corona
"Kwa sasa tunaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupambana na janga hili la Corona. Tupo tayari kwa maamuzi yoyote yatayochukuliwa, tumejipanga kumaliza msimu vizuri," amesema
Aidha Mwakalebela amefafanua kilichoelezwa na gazeti moja la kila siku kuwa alipendekeza ligi ifutwe na Simba ipewe ubingwa
"Mimi sikutoa kauli hiyo, mwandishi alitumia maneno ya mtu mwingine kuniwekea mimi. Nadhani lengo lake lilikuwa kuuza habari yake. Sisi msimamo wetu kama Yanga tuko pamoja na maamuzi ya Mamlaka husika. Kwa sasa ligi imesimama, tunatambua usalama wa watu ni muhimu zaidi lakini mimi sikusema wafute ligi"
"Tumejipanga kufanya vizuri kwenye mechi zilizobaki pale ligi itakaporejea lakini pia tumejipanga kuhakikisha tunashinda taji la FA"