Mshambuliaji wa Yanga David Molinga amesema amepokea ofa kutoka vilabu mbalimbali ambavyo vinataka huduma yake
Mcongomani huyo ni kama amepoteza mvuto kutoka kwa mashabiki wa Yanga licha ya ukweli ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi cha timu hiyo
Molinga amefunga mabao nane kwenye ligi
Licha ya kuwa na ofa hizo mkononi, Molinga amesema kabla ya kufanya maamuzi, atawapa kipaumbele Yanga ambao ndio waaajiri wake wa sasa
"Bado nina mkataba hapa mpaka mwezi Agosti lakini ninazo barua za ofa kutoka timu nyingine. Nimeitwa Tunisia klabu Etoile Du Sahel ambako nimepewa mwaliko wa kufanya majaribio kwa siku 15," amesema
"Lakini pia kuna timu nyingine Union Cidi Kasem imenipa ofa ya mkataba moja kwa moja. Nasubiri kuwataarifu mabosi wangu (Yanga) kuhusu ofa hizi na pengine baada ya changamoto hii ya corona kupita, naweza kuondoka"
"Nimeishi vizuri hapa Yanga, sitapenda kuondoka kabla ya kuwasikiliza mabosi wangu. Hivyo kama watanihitaji, nitakuwa tayari kusaini mkataba mpya"
Molinga ni miongoni mwa wachezaji ambao inadaiwa kocha Luc Eymael amependekeza apewe mkono wa kwaheri