Mkufunzi wa Yanga Luc Eymael amewaahidi mashabiki wa timu hiyo kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Eymael ambaye kwa sasa yuko mapumziko Ubelgiji, amekiri Simba kutoshikika kwenye mbio za ubingwa msimu huu, kwani wako mbali kwa pointi na idadi ya michezo waliyobaki nayo, wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.
Simba kwa sasa inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 71, nafasi ya pili Azam FC wenye pointi 54 wote wakicheza michezo 28 wakati Yanga wamecheza mechi 27 wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 51.
Eymael alisema kwa sasa mipango yake anaielekeza kusajili wachezaji wenye uwezo zaidi wa kushindana na tayari baadhi ya nyota wa timu hiyo wameshaongezewa mikataba.
"Nawaomba mashabiki kwa sasa hatuwezi kutumia nguvu kubwa kupigania ubingwa, kwani Simba wana nafasi kubwa ya kutwaa, lakini tujiandae kwa msimu ujao ubingwa ni wetu, "alisema Eymael.
Eymael anatarajia kurejea nchini Aprili 5 akitokea kwao Ubelgiji alikokwenda kufunga ndoa alisema alishaongea na mdhamini wao GSM na kumaliza kila kitu kwa kuwapatia majina ya wachezaji ambao anataka waongezwe mikatana na wale wa kuwasajili upya.
Alisema Bernard Morrisoni na Papy Tshishimbi ni miongoni mwa majina ya wachezaji aliyowasilisha kwenye meza ya mdhamini huyo ili kuwaongezea mikataba haraka katika kipindi hiki, ambacho timu nyingi zinaweza kutumia nafasi hiyo kufanya mazungumzo nao.