Kinara wa mabao Yanga, mshambuliaji David Molinga siku zake ndani ya klabu hiyo zimeanza kuhesabika
Mshambuliaji Molinga amefunga mabao manane hadi sasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini maisha yake ndani Yanga yamekuwa njia panda tangu kutimuliwa kwa kocha Mwinyi Zahera.
Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amekabidhi ripoti yake akianisha wachezaji anaotaka kuwa nao kwa msimu ujao pamoja na wale wa kuachwa au kutolewa kwa mkopo.
Inaelezwa katika ripoti iliyoachwa na Eymael, jina la Molinga ni miongoni mwa wachezaji aliopendekeza wapewe mkono wa kwaheri
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alipoulizwa juu ya kuachana na mchezaji huyo alisema kila mchezaji ambaye kocha amependekeza aachwe hata kama ana mkataba na Yanga basi ataachwa.
"Ripoti ya kocha bado iko kwenye kamati ya ufundi, lakini ukweli huko hivi, mchezaji ambaye kocha amependekeza asajiliwe atasajiliwa, wa kuachwa ataachwa na wa kutolewa kwa mkopo itakuwa hivyo," Mwakalebela amenukuliwa na mtandao wa Mwanaspoti
Tangu atue Yanga mwanzoni mwa msimu, Molinga amekumbana na mikasa ya hapa na pale inayohusiana na masuala ya utovu wa nidhamu
Yanga ilimsajili Molinga kwa mkopo, akipewa mkataba wa mwaka mmoja, hivyo haitaingia hasara yoyote ikiamua kuachana nae