Uongozi wa Yanga jana ulivunja kambi na kuwaruhusu wachezaji kurudi makwao kufuatia uamuzi wa Serikali kusimamisha shughuli zote za michezo kwa siku 30 baada ya ugonjwa wa Corona kuingia nchini
Baada ya mazoezi jana asubuhi, Mkufunzi wa Yanga Luc Eymael aliwaandalia wachezaji program binafsi za mazoezi ambazo wanapaswa kuzitekeleza huko majumbani kwao
Mbelgiji huyo amewasisitizia wachezaji kuwa ni lazima wakamilishe program hizo na atakuwa akiwafuatilia
Mara nyingi wachezaji wanapokuwa majumbani, baadhi huwa wazito kufanya mazoezi jambo ambalo linaweza kuwarejesha nyuma
"Nimempa kila mchezaji program ya mazoezi ambayo atapaswa kufanya mwenyewe.
"Nitawafuatilia mara kwa mara kupitia mawasiliano yao ili kuhakikisha wanatekeleza.
"Tuna mechi muhimu za kumalizia msimu, pamoja na kuwa tumepoteza nafasi ya kutwaa ubingwa, lakini tunahitaji kupambana angalau tumalize nafasi ya pili. Lakini pia tuna michuano ya kombe la Shirikisho ambayo ni muhimu sasa kwetu," alisema Eymael
Wachezaji watarejea mazoezini April 17 baada ya siku 30 zilizotolewa na Serikali kumalizika