Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Heritier Makambo, amesema anatamani kurejea Jangwani kukitumikia kikosi hicho, akivutiwa na kiwango kinachoonyeshwa na Bernard Morrison aliyetokea kuwa kipenzi cha Wanayanga kwa sasa.
Katika kuonyesha jinsi alivyovutiwa na Morrision, Makambo amewataka viongozi wa Yanga kuangalia ni vipi wanaweza kumrejesha Jangwani ili je kuwapa raha mashabiki wa timu yake hiyo ya zamani kwa kupiga mabao kama mvua.
Katika mahojiano na gazeti la Bingwa, Makambo alisema kwa jinsi anavyomuona Morrison, anaamini akicheza naye watajenga kombinesheni ya hatari itakayokuwa kilio kwa timu pinzani.
Alisema uzuri ni kwamba anaipenda mno Yanga na anatamani mno kuichezea tena timu hiyo iwe ni kabla au baada ya kumaliza mkataba wake Horoya.
"Yanga ipo damuni mwangu, huwa ninaifuatilia sana na katika kikosi cha sasa, naona kina wachezaji wengi wazuri ambao wakipata muda wa kukaa pamoja zaidi, wataisaidia sana timu.
"Kati ya wachezaji walionivutia, kuna Morrison, ni mchezaji mzuri sana, natamani sana kucheza naye pamoja, naamini kama nikirudi Yanga na akiendelea kuwepo kikosini, watanikoma, nitafunga mabao kila mchezo na kuwapa raha mashabiki wa Yanga," alisema Makambo.
"Nimebakiza miaka miwili katika mkataba wangu kwani nilisaini miaka mitatu, lakini kama Yanga wakitaka wanaweza kuja kuzungumza na mabosi wangu huku ili nirudi Tanzania."
Makambo alisema kwa vyovyote itakavyokuwa, katika akili yake, Yanga anaipa nafasi ya kwanza ikitokea ameondoka Horoya, labda kama Wanajangwani hao hawatamuhitaji.
Yanga ilimuuza Makambo katika kikosi cha Horoya msimu uliopita, ikiwa ni baada ya straika huyo raia wa DRC kuisaidia mno timu hiyo, akiwa ni moto wa kuotea mbali katika kufunga mabao.