Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ameeleza kuvutiwa na kiwango cha kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye tangu amrejeshe kikosi cha kwanza kiwango chake kiko juu
Eymael amemtumia Fei Toto kwenye michezo dhidi ya Alliance Fc na Mbao Fc ambapo fundi huyo wa mpira alionyesha kiwango cha hali ya juu
Jana katika mchezo dhidi ya Mbao Fc, Eymael alimchezesha Feisal namba nane na ndiye aliyesababisha mkwaju wa penati uliofungwa na David Molinga
Mbelgiji huyo alisema Fei Toto ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu lakini msimu huu hakuwa akifanya vizuri kutokana na kukabiliwa na changamoto ndogo ndogo
Hata hivyo amesema baada ya changamoto hizo kumalizika, Fei Toto ameanza kuonyesha makali yake
Eymael amesema kama nyota ataendelea kubaki kwenye kiwango chake alichonacho sasa, Wanayanga watarajie mambo makubwa kutoka kwake
"Feisal ni mchezaji mzuri sana na ana kipaji kikubwa pia, ukimuangalia mazoezini basi utamgundua ni mchezaji wa aina gani, kuna vitu vidogo sana vilikuwa vinamfanya ashindwe kufanya vizuri, nadhani kwa sasa vimemalizika na unaona jinsi ambavyo amecheza vizuri, hakika natamani acheze hivi kila siku," alisema Eymael
Fei Toto huenda akajumuishwa kwenye kikosi kitakachoikabili Simba siku ya Jumapili, hata hivyo Eymae anakabiliwa na changamoto ya kuchagua kikosi chake cha kwanza kutokana na ubora wa nyota wake hasa sehemu ya kiungo
Feisal Salum, Haruna Niyonzima, Papy Tshishimbi, Mapinduzi Balama na Mohammed Issa 'Banka' wote wanafanya vizuri