Yanga imeendelea kutakata uwanja wa Taifa baada ya kuichapa Mbao Fc mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Huo ni ushindi wa pili mfululizo Yanga inapata kwenye ligi na wa tatu katika mashindano yote
Mabao ya Yanga yalifungwa na David Molinga (mkwaju wa penati) na Patrick Sibomana 'PS'
Molinga alifunga bao lake la nane msimu huu kwenye dakika ya 28 baada Feisal Salum kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kutoa mkwaju wa penati kwa Yanga
Bao hilo lilidumu mpaka wakati wa mapumziko
Kipindi cha pili mabingwa hao wa kihistoria waliendelea kuwapeleka 'mpera-mpera' Mbao Fc, kukosekana kwa umakini kwenye safu ya ushambuliaji kuliinyima Yanga nafasi ya kuondoka na ushindi mnono
Baada ya kosa kosa nyingi, Sibomana aliongeza bao la pili kwenye dakika ya 81 akimalizia pasi murua ya Tariq Seif
Hilo lilikuwa bao la tano kwa Sibomana ambaye alirejeshwa kikosini kwa mara ya kwanza baada ya kukosekana kwa wiki kadhaa
Ushindi huo umeiweka Yanga sawa kuelekea mchezo dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumapili, March 08
Kocha Luc Eymael leo alifanya mabadiliko ya kikosi chake kilichoanza akiwaweka nje Haruna Niyonzima mwenye kadi mbili za njano, Ditram Nchimbi, Jaffar Mohammed, Metacha Mnata huku akiwarejesha Ngasa, Molinga na Sibomana