Uongozi wa klabu ya Yanga umesema kuwa unatambua machungu wanayopata mashabiki wao kutokana na timu kutofanya vizuri katika michezo ya hivi karibuni
Akizungumza na wanahabari mapema leo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema viongozi walikutana na kufanya tathmini ya mwenendo wa timu na sasa wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo yote inayokuja wakianza na mchezo wa kombe la FA dhidi ya Gwambina FC ambao utapigwa kesho Jumatano kwenye uwanja wa Taifa
"Sisi ni klabu ya mpira, malengo yetu ni kushinda, hapa kati naweza kusema ni kama upepo mbaya ulipita lakini tumeliona tatizo na tunawaahidi Wanayanga tutarejea kivingine"
"Tuna timu nzuri, benchi la ufundi zuri. Viongozi tutaendelea kutimiza wajibu wetu, wachezaji na benchi la ufundi watatimiza wajibu wao na hata kwa upande wa mashabiki tunaomba iwe hivyo
"Tunawaomba waendelee kuiunga mkono timu yao kwani kila kitu kitakuwa sawa"
Aidha katika jitihada za kuongeza hamasa ya timu, uongozi wa Yanga umetangaza kurejea kwa aliyewahi kuwa Afisa habari wa timu hiyo Jery Muro ambaye amerejea kufanya kazi ya hamasa kama shabiki wa Mwanachama mwaminifu wa Yanga
Muro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, amesema kwa sasa yuko likizo na ameamua kuitumia likizo yake kuongeza nguvu kuelekea mchezo dhidi ya Simba ambao utapigwa march 8