Timu ya Yanga imetua jijini Tanga na kufanya kufuru ya aina yake, kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union unaotarajiwa kuchezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo, Yanga wamejichimbia katika hoteli ya bei mbaya ambayo ndiyo inayotumiwa na wageni maarufu, kuanzia viongozi wa serikali, wasanii na wengineo.
Hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tano, ni Tanga Beach Resort iliyopo ufukweni wa Bahari ya Hindi.
Sambamba na hilo, mashabiki wa timu ya African Sports ya jijini Tanga, wenye ‘undugu’ wa kiasili na Yanga, wameamua kuungana na Wanajangwani hao ili kuwapa njia za kuwawezesha kuifunga Coastal Union.
Ikumbukwe Yanga na African Sports zina uhusiano wa kiasili, huku Coastal Union maswahiba wao wakiwa ni Simba.
Mara baada ya kikosi cha Yanga kutua Tanga, ilikutana na mapokezi ya aina yake kutokana na umati mkubwa wa mashabiki na wanachama wao waliojitokeza kuwalaki vijana wao.
Tayari shamrashamra za kuelekea mchezo huo zimeanza huku wauzaji wa jezi wakiwa tayari wamekwisha kuanza kufanya yao katika mitaa mbalimbali ya jiji hili.
Na jana jioni, kikosi cha Yanga kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Popatlaly, chini ya kocha wao, Luc Eymael.

Mazoezi hayo yalifanyika chini ya ulinzi mkali, yakihudhuriwa na mashabiki lukuki, huku baadhi wakizuiwa kuingia uwanjani hapo, ikiwa ni moja ya sehemu ya joto la mchezo huo wa Jumapili.
Akiuzungumzia mchezo huo, Eymael alisema:
"Tunacheza na timu nzuri, Coastal Union imepoteza mechi yao iliyopita na walikuwa na matokeo mazuri, hivyo wamejipanga. Lakini nasi tumejipanga kuchukua pointi tatu. Mechi iliyopita tulipata sare, hivyo tuna kila sababu ya kushinda mechi hii."