Starika kinara wa mabao wa Kagera Sugar, Yusuf Mhilu amesema hakuna kitu kinachomuumiza kama alipotolewa Yanga na kupelekwa Ndanda FC ambapo, jambo hilo lilimfanya awe na hasira ndio maana leo amekuwa moto mkali.
Mhilu amesema alipotolewa Jangwani aliona kama amerudishwa nyuma, lakini akatuliza akili yake na kujipanga na leo amekuwa mmoja ya mastraika hatari nchini kwa kucheka na nyavu.

Mhilu aliyeanza kuichezea Yanga B kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa mwaka 2017, amesema ndoto yake kubwa ilikuwa kuonekana na timu za nje, lakini mambo hayakwenda alivyotaka kupitia Yanga.
Amesema mwishoni mwa msimu wa 2018/19 Yanga ilimpeleka kwa mkopo Ndanda, kitu anachokiri kilimuumiza nakuona badala ya kusonga mbele anarudi nyuma.
"Sio aibu kwa mchezaji kutoka Simba, Yanga na Azam FC kwenda timu za mkoani, lakini imejengeka mazoea mchezaji wa hivyo ni anaonekana kama alikosa malengo ya kucheza nje kwani timu hizo zina nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa hivyo inakuwa ni nafasi kwetu kuonekana," amesema Mhilu na kuongeza;
"Nilipanda Yanga ikiwa na washambuliaji wazoefu hivyo ikawa ngumu kuaminiwa moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, ndio maana ikanitoa kwa mkopo kwenda Ndanda FC, na hiyo ilinifanya nipambane ili kupata timu iliopo nafasi za juu kwenye Ligi Kuu na bahati ikaniangukia Kagera Sugar."
Amesema kwa sasa ameweza kubaini kuwa, kuondoka kwake Yanga kumemsaidia tofauti na alivyokuwa akifikiri mwanzoni, kwani hasira alizokuwa nazo zimemfanya awe mkali kiasi kwamba kwa sasa naye yupo kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu.
"Hasira zangu kwa Yanga kunitoa kwa mkopo zimenijengea ujasiri na kujiamini ili kutaka kuthibitisha kuwa, mie ni mmoja ya wachezaji wenye vipaji na ambao wenye uwezo wa kupambana, naamini ningebaki Jangwani huenda nisingefika hapa nilipo"
Mhilu ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi cha Kagera Sugar akiwa amefunga mabao tisa