Pamoja na kocha Luc Eymael kuelekeza kubaini mapungufu ya mshambuliaji Yikpe Gislaim na kuahidi kumuimarisha, uvumilivu ni kama umeanza kuwashinda baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao wametaka mkataba wa mchezaji huyo uvunjwe
Eymael jana alimuanzisha Yikpe kwenye kikosi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao ulimalizika kwa suluhu ya bila ya kufungana
Hata hivyo mshambuliaji huyo hakuwa na mchezo mzuri
Baada ya mchezo kumalizika, baadhi ya mashabiki waliojitokeza uwanja wa Taifa kushuhudia mtanange huo, walimvaa msemaji wa Yanga Antonio Nugaz wakieleza kutofurahishwa na kiwango cha mchezaji huyo
Aidha mashabiki hao walidai kuwa ni bora wangemrudisha Mrundi Amissi Tambwe kuliko kuendelea kuwa na wachezaji ambao wanalipwa mishahara mikubwa halafu hawana msaada kwa timu
"Kwa kweli hapa kwa Yikpe uongozi wa Yanga hauwezi kukwepa lawama kwani haonekani kuwa na uwezo wa kuisaidia Yanga"
"Wanasema apewe muda lakini sidhani, hakuna na muda ambao utamtosha kuonyesha uwezo wake, mbona Morrison alipokuja alionyesha ubora kwenye mchezo wake wa kwanza? Ni bora hata uongozi ungemrudisha Tambwe tu," alisikika mmoja wa mashabiki hao
Tangu atue Yanga kutoka klabu ya Gor Mahia, Yikpe amefunga mabao mawili, moja kwenye ligi dhidi ya Singida United na jingine kwenye kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons
Kocha wa Yanga Luc Eymael amesema Yikpe ni mshambuliaji mzuri lakini ana mapungufu madogo ambayo amesema yanaweza kurekebishwa
Aidha Eymael aliongeza kuwa kwa sasa wanapaswa kuwatumia washambuliaji waliopo hadi mwishoni mwa msimu kwani dirisha la usajili lilishafungwa