Mkufunzi wa Yanga Luc Eymael amekiri kuwa mshambuliaji wake mpya Bernard Morrison anakamiwa sana na mabeki wa timu pinzani jambo linalompa wakati mgumu kwenye baadhi ya mechi
Hata hivyo Eymael amesema anafahamu jinsi ya kumtumia mshambuliaji huyo ili kuinufaisha Yanga
"Timu pinzani wanamkamia sana Morrison, wanamfanyia madhambi kila mara. Tumebaini hilo, wakati mwingine tutakuja tofauti, hawataamini" amesema
Tangu ajiunge na Yanga, Morrison amekuwa gumzo kutokana na umahiri wake dimbani
Pengine hii ndio sababu inayofanya timu pinzani kumuwekea ulinzi maalum kwenye kila mchezo dhidi ya Yanga
Lakini bado ameendelea kun'gara, mchezo uliopita akifunga bao pekee la Yanga kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City
Mpaka sasa Morrison amefunga mabao mawili na kutoa pasi tatu za mabao
Ikumbukwe bado hajamaliza hata mwezi tangu alipojiunga na Yanga siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo
Lakini ni mchezaji ambaye mchango wake unaweza kudhani yuko Yanga tangu msimu uliopita