Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael amembadilishia majukumu mshambuliaji Ditram Nchimbi ambapo sasa anatumika kama winga licha ya kusajiliwa akiwa mshambuliaji wa kati
Eymael alitaja sababu ya kumtumia Nchimbi pembeni ni kuwa amebaini mchezaji huyo mpambanaji, ana kasi, uwezo mzuri wa kumiliki mpira na umahiri wa kupiga krosi
Amesema baada ya kumjaribu kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, amejiridhisha kuwa atakuwa na msaada mkubwa kwa timu kama akicheza pembeni kuliko akiwa mshambuliaji wa kati
Takwimu za Nchimbi katika mechi mbili alizocheza kama winga, zinadhihirisha kile alichosema Eymael
Akitokea pembeni ametoa pasi mbili za mabao ambayo yote yalifungwa na David Molinga katika michezo dhidi ya Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting
Aidha Nchimbi maarufu kama Duma, amekuwa akipiga krosi nyingi ambazo zinasababisha kashkash lango la timu pinzani
Molinga anaweza kunufaika zaidi na krosi hizo kama ataongeza umakini
Halikuwa jambo la kushangaza Nchimbi kuchaguliwa kuwa nyota wa mchezo juzi kutokana na uwezo alioonyesha
Pacha yake na Molinga inanoga
Molinga na Nchimbi ni kama wameanza kuzoeana huku kila mmoja akimsoma vyema mwenzake
Wakati Nchimbi akiwa na mpira pembeni mara nyingi anaangalia eneo analokuwa Molinga ambaye ni hodari wa kupiga mipira ya vichwa na hata mipira ya chini

Mechi dhidi ya Ruvu Shooting Molinga angeweza kufunga mabao zaidi kama angetumia vyema nafasi alizotengenezewa na Nchimbi
Kama kocha ataendelea kuwatumia wawili hao pamoja, huenda baadae wakatengeneza pacha hatari ya kupachika mabao Yanga