Mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga wameendelea kutakata baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Uhuru
Alikuwa ni David Molinga aliyeihakikishia Yanga ushindi muhimu baada ya kuifungia bao pekee kwenye dakika ya 40 kwa kichwa
Molinga aliitendea haki krosi maridhawa aliyochongwa na Ditram Nchimbi kutokea upande wa kulia
Hilo ni bao la pili wawili hao wanahusika, ni kama nakala ya bao walilofunga kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar
Yanga ilikuwa bora sana kwenye kipindi cha kwanza na ingeweza kufunga mabao zaidi kama nyota wake wangetumia nafasi nyingi walizotengeneza
Katika kipindi hicho pia Yanga ilinyimwa mkwaju dhahiri wa penati baada ya Bernard Morrison kuangushwa ndani ya eneo la hatari lakini mwamuzi akaamuru ipigwe kona licha ya kuwa mpira ulitolewa na Morrison baada ya kuangushwa
Kipindi cha pili Yanga ilipunguza kasi na kuwapa nafasi Ruvu Shooting kurejea mchezoni
Hata hivyo umakini wa safu ya ulinzi ambayo leo ilikuwa chini ya uongozi wa Lamine Moro na Ally Mtoni, pamoja na mlinda lango Metacha Mnata, waliweza kuhakikisha Yanga inaondoka na alama zote tatu